Wizara ya Nishati na Madini inapanga kushirikiana na Kampuni ya Mitsubishi Hitachi Power System ya Japan katika kuendeleza sekta ya nishati nchini.
Rais wa Kampuni ya Mitsubishi Hitachi Power System Ltd, Takato Nishizawa (Kulia), akitoa ufafanuzi kuhusu shughuli zinazofanywa na Kampuni yake kwa Wataalamu wa Wizara ya Nishati na Madini (Kushoto), wakati wa Kikao kilichokutanisha pande hizo mbili Makao Makuu ya Wizara jijini Dar es Salaam, Mei 12, 2015 kwa lengo la kujadili ushirikiano katika sekta ya nishati.
Kamishna Msaidizi wa Umeme wa Wizara, Mhandisi Innocent Luoga aliyasema hayo mapema leo baada ya kukutana na uongozi wa juu wa kampuni hiyo, Makao Makuu ya Wizara jijini Dar es Salaam.
Mhandisi Luoga alisema katika kikao hicho, Ujumbe wa kampuni ya Mitsubishi Hitachi Power Systems Ltd uliwasilisha mapendekezo ya matumizi ya teknolojia ya kisasa ya kufua umeme kutokana na vyanzo mbalimbali ikiwemo makaa ya mawe, jotoardhi na gesi.
Wataalamu wa Wizara ya Nishati na Madini (Kushoto) wakiwa katika Kikao na Wataalamu wa Kampuni ya Mitsubishi Hitachi Power System Ltd (Kulia). Kikao kilijadili kuhusu ushirikiano katika sekta ya nishati na kilifanyika Mei 12, 2015 Makao Makuu ya Wizara, Dar es Salaam.
“Sisi kama Serikali, kupitia taasisi zetu tumeona ni vema tushirikiane na Kampuni hii ambayo inajishughulisha na kutengeneza mitambo ya kufua umeme wa gesi, makaa ya mawe na jotoardhi kwa kutumia teknojia ya kisasa. Hii ni kutokana na vyanzo vipya vya umeme tulivyonavyo hususan makaa ya mawe na jotoardhi, ambavyo hatujaanza rasmi kuvitumia kuzalisha umeme,” alisema Kamishna Luoga.
Aliongeza kuwa, lengo la Serikali ni kuhakikisha umeme wa kutosha, wa uhakika na wa bei nafuu unazalishwa na kusambazwa nchini ili kuwaletea wananchi maendeleo na hivyo kuinua pato la Taifa kwa ujumla.
Makamu Rais wa Kampuni ya Mitsubishi Hitachi Power System Ltd, Satoshi Uchida (Kulia), akifafanua jambo kwa Wataalamu wa Wizara ya Nishati na Madini, wakati wa kikao baina yao kilichojadili ushirikiano katika sekta ya nishati. Kikao kilifanyika Mei 12, 2015 Makao Makuu ya Wizara jijini Dar es Salaam.
Alisema kuwa, Kampuni hiyo ilishafanya majadiliano kuhusu ushirikiano katika sekta ya nishati na taasisi zilizo chini ya Wizara ambazo ni Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) pamoja na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).
Akizungumzia kuhusu faida za matumizi ya teknolojia hiyo ya kisasa inayotumika kufua umeme, Kamishna Luoga alizitaja kuwa ni pamoja na kuwa rafiki wa mazingira, kuwezesha uhakika wa kufua umeme kwa bei nafuu pamoja na kufua umeme kwa ufanisi mkubwa.
Rais wa Kampuni ya Mitsubishi Hitachi Power System Ltd, Takato Nishizawa (Kulia), akitoa ufafanuzi kuhusu shughuli zinazofanywa na Kampuni yake kwa Wataalamu wa Wizara ya Nishati na Madini (Kushoto), wakati wa Kikao kilichokutanisha pande hizo mbili Makao Makuu ya Wizara jijini Dar es Salaam, Mei 12, 2015 kwa lengo la kujadili ushirikiano katika sekta ya nishati.
Awali, katika kikao hicho baina ya Wizara na Kampuni hiyo, Rais wa Kampuni, Takato Nishizawa alisema kampuni yake iko tayari kutoa mafunzo ya namna ya kutumia mitambo yao inayotumia teknolojia hiyo ya kisasa kwa Wahandisi wa kitanzania.
Aidha, Nishizawa alitoa mwaliko kwa wataalamu hao kutoka Tanzania, kutembelea mitambo hiyo huko Japan kwa lengo la kujifunza zaidi.
Katika hatua nyingine, ilielezwa kuwa Kampuni ya Mitsubishi Hitachi Power System Ltd, tayari imeingia mkataba na Kampuni ya Sumitomo ambayo inatekeleza Mradi wa Kufua Umeme wa gesi wa Kinyerezi II unaofikia kiasi cha Megawati 240, kwa kazi ya kufunga mitambo ya kufua umeme (gas turbines) aina ya Hitachi.