Awali kambi hiyo, ambayo ni kumbwa zaidi duniani, ilikuwa imepangwa kufungwa mwishoni mwa mwaka huu lakini sasa muda huo umerefushwa hadi mwezi Mei mwaka ujao wa 2017.
Kambi ya wakimbizi ya Dadaab iko katika eneo kavu la kaskazini mashariki mwa Kenya na ni makao ya watu zaidi ya laki tatu ambapo aghalabu yao ni raia wa nchi jirani ya Somalia inayokumbwa na vita.
Katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na kushadhidi vita katika maeneo mbali mbali ya Somalia hasa hujuma za magaidi wa Al Shabab, idadi kubwa ya Wasomali wamekimbilia hifadhi katika kambi hiyo ya Daadab.
Kwa mujibu wa takwimu, idadi ya wakimbizi wanaoishi nchini Kenya ni 623,000 na aghalabu yao wako katika kambi ya Dadaab na ile ya Kakuma iliyo eneo la kaskazini karibu na mpaka wa nchi hiyo na Sudan Kusini.